KARIBUNI KWENYE BLOG YANGU ILI USIPITWE NA HABARI KEMKEM,KWA HABARI MOTOMOTO NDANI NA NJE YA NCHI MICHEZO NA BURUDANI NA ZINGINEZO NYINGI UNGANA NAMI NICK 4REAL

Friday, June 27, 2014

HIVI NDIVYO UWANJA WA TAIFA UMAOFAGILIWA BRAZIL

Uwanja wa Taifa wa Tanzania unaosifiwa na watu wa Brazil kuwa una ubora wa Kimataifa. Picha na Maktaba 

Kwa ufupi
Televisheni maarufu ya Globo Sports ya Brazil ilionyesha moja kwa moja mechi hiyo na kitu pekee kilichowakosha zaidi ni uwanja wetu wa kisasa. Wengi hawakumbuki vizuri matokeo wala wafungaji wa pambano hilo kwa sababu hawakulitilia maanani sana, lakini wanakumbuka kwamba Tanzania ina uwanja mzuri.

Huo uwanja ambao tunaung’oa viti hapo Temeke kwa vurugu zisizo na msingi kumbe ni gumzo Brazil. Huo uwanja ambao Watanzania hatuoni thamani yake na tunadhani ni uwanja mzuri wa kawaida tu kumbe ni gumzo Brazil.

Kumbe mashabiki wa Brazil walipata fursa ya

kulitazama pambano kati ya Taifa Stars na Brazil lililochezwa katika uwanja wetu huo wa Taifa Juni 2010, wakati Brazil wakiwa njiani kushiriki michuano ya Kombe la Dunia nchini Afrika Kusini.

Televisheni maarufu ya Globo Sports ya Brazil ilionyesha moja kwa moja mechi hiyo na kitu pekee kilichowakosha zaidi ni uwanja wetu wa kisasa. Wengi hawakumbuki vizuri matokeo wala wafungaji wa pambano hilo kwa sababu hawakulitilia maanani sana, lakini wanakumbuka kwamba Tanzania ina uwanja mzuri.

"Sijui tuliwafunga saba au sita, lakini mna uwanja mzuri kweli kweli. Kwanini hamchezi mechi za kimataifa? Nani alijenga uwanja ule? Sehemu nyingine za Afrika achilia mbali Afrika Kusini kuna viwanja kama vile?" Anahoji Almelda Oliveira, shabiki mzuri wa timu ya taifa ya Brazil, Selecao.

Kituko nilikutana nacho katika treni wakati natokakutazama pambano la Urusi na Ubelgiji. Shabiki mmoja wa Brazil alidai kwamba Watanzania waliwapa Wachina dhahabu nyingi kwa ajili ya kujenga huu uwanja.

"Niliuona uwanja huo. Watanzania waliwapa Wachina dhahabu nyingi kwa ajili ya kuwajenga ule uwanja. Nchi maskini kama Tanzania haiwezi kuwa na uwanja kama ule," alisema kwa kujiamini shabiki mmoja ambaye hakutaka kujitambulisha jina.

Hata hivyo, shabiki huyo alionekana kuungana na mawazo ya watu wanaoandamana nchini hapa, ambao wanaamini kuwa serikali yao imetumia fedha nyingi kujenga viwanja, lakini Tanzania ilifanya biashara ya kubadilishana.

"Hapa serikali imetumia fedha za walipa kodi, Tanzania ilibadilishana dhahabu na uwanja. Nyie ni maskini hamuwezi kujenga uwanja ule kwa fedha za walipa kodi," alidai shabiki huyo ambaye mwishowe alishukia katika kituo cha Botafogo.

Shabiki mmoja aliyeulizwa kama anaufahamu uwanja wa Taifa (Tanzania), alidai kwamba anakumbuka kuwa Brazil ilicheza katika uwanja mmoja mzuri barani Afrika wakati wakijiandaa na michuano ya Kombe la Dunia 2010.

Hakumbuki kama ilikuwa ni katika pambano dhidi ya Zimbabwe au Tanzania, lakini anachokumbuka ni kwamba ulikuwa uwanja mzuri na wa kisasa.

Joan Silva, muuza duka katika Mtaa wa Rui Aurora, anadai kwamba ni matumizi mabaya ya fedha kuwa na uwanja mzuri kama wa taifa halafu timu yenyewe isiwe inashiriki michuano yoyote ya maana.

“"Mmewahi kushiriki Kombe la Dunia? Najua bado. Sasa kwanini mna uwanja kama ule wakati mnajua wazi kwamba hamna timu nzuri. Nakumbuka tuliwafunga mabao matano," alisema Silva, ambaye ni rafiki kipenzi cha Watanzania wanaoishi Sao Paulo.

Watanzania  ambao wameondoka nchini kwa muda mrefu pia wameshangazwa na uzuri wa Uwanja wa Taifa. China Keya, kiungo wa zamani wa Pan Afrika na timu ya Mkoa wa Dar es salaam 'Mzizima', ambaye ameishi Brazil kwa miaka 13 ni mmoja kati ya watu walioshangazwa na ubora wa Uwanja wa Taifa.

 

"Uwanja ni mzuri sana. Tulitazama moja kwa moja mechi yetu na Wabrazil na hata mimi mwenyewe nilishangazwa na uwanja wetu. Kilichonishangaza zaidi ni nyasi zake. Zamani wakati sisi tunacheza ule uwanja wa zamani nyasi zilikuwa mbovu sana.

"Achilia mbali uwanjani, Wabrazil walionyesha fukwe zetu ikiwemo Coco pamoja na eneo kubwa la bahari. Wabrazil wanapenda sana bahari na siku zote kwa ujinga wao wanaamini kwamba bahari iko Brazil tu. Wakienda nchi nyingine wanashangaa kukuta bahari," anasema China.

Mtanzania mmoja ambaye hakutaka kutaja jina lake alidai kuwa alitazama pambano hilo akiwa jela nchini Brazil na raia wa nchi za Afrika Magharibi za Senegal, Nigeria na Ivory Coast walikuwa wameushangaa uwanja vilivyo.

"Wanigeria, Wasenegal, Ivory Coast na wengineo walikuwa wanashangaa kuona uwanja kama ule uko Tanzania. Hawakutegemea. Nashangaa kusikia kuna baadhi ya Watanzania wanang'oa viti katika uwanja kama huo,"alisema Mtanzania huyo ambaye ameomba jina lake lihifadhiwe.

Brazil ina viwanja vizuri ambavyo gharama zake ni kubwa kuliko Uwanja wa Taifa. Viwanja kama Mane Garincha, Maracana na vinginevyo, lakini unapoona kuwa mashabiki wa nchi mbalimbali wakitambua uzuri wa Uwanja wa Taifa ni wakati wa kuhoji mashabiki wanaong'oa viti. Aibu juu yao!

SOURCE HABARI KWANZA

No comments :

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...