Kwa nyakati tofauti juzi na jana NIPASHE ilikuwa ikiwauliza viongozi mbalimbali wa shirikisho hilo kama kuna uwezekano wa kuanza kutumika kwa mfumo huo kesho lakini hawakuwa tayari kueleza kinachoendelea.
"Kwa sasa (juzi saa 7:13 mchana) sijaelezwa chochote kuhusu maendeleo ya ufungaji wa vifaa kwenye viwanja. Lakini viwanja vilivyokuwa vimebaki ni Ali Hassan Mwinyi na Uwanja wa Taifa. Mtafute Mwenyekiti wa Kamati ya Ligi (Wallace Karia), suala hili linamhusu," alisema Afisa Habari wa TFF, Boniface Wambura.
Alipotafutwa na mwandishi juzi mchana Karia alisema: "Mimi niko Morogoro na sijui kinachoendelea kuhusu tiketi za elektroniki. Leo (juzi) kulikuwa na kikao cha TFF, CRDB na serikali kuhusu suala hilo. Muulize Kawemba (Mkurugenzi wa Mashindano wa TFF) kwa sababu ndiye aliyeliwakilisha shirikisho katika kikao hicho."
NIPASHE ilimpigia simu Kawemba juzi lakini simu yake ya mkononi ilikuwa ikiita bila kupokewa. Jana saa 9:08 alasiri Kawemba aliliambia gazeti hili kuwa watatoa tamko rasmi kuhusu suala hilo leo.
"Ni kweli jana (juzi) tulikuta na CRDB na serikali kuzungumzia suala hilo.
Mimi kama afisa wa TFF anayeshughulikia suala hilo nimeshakabidhi kwa msemaji wa shirikisho (Wambura) yale tuliyojadili kwenye kikao na kesho (leo) atawaeleza waandishi wa habari.
Jana jioni gazeti hili lilimtafuta Wambura ambaye alikiri kupokea taarifa ya kikao hicho na kuahidi kutoa ufafanuzi kwa wanahabari leo mchana kwenye makao makuu ya shirikisho hilo jijini Dar es Salaam.
KWA NINI ELEKTRONIKI
Kimsingi, tiketi za elektroniki zilipaswa kuanza kutumika katika mzunguko wa pili wa msimu uliopita kama ilivyokuwa imeahidiwa na Rais wa TFF, Leodegar Tenga.
Mwaka juzi shirikisho hillo ilitangaza ‘tenda' ya kutengeneza tiketi za kielektroniki kwa ajili ya mechi za klabu na timu za taifa na benki ya CRDB ndiyo iliyoshinda zabuni.
Kutangazwakwa zabuni hiyo kulitokana na ripoti ya Mei 2011 ya Kamati Maalum ya Kudhibiti na Kuboresha Mapato ya TFF iliyopendekeza kuachwa mara moja kutumika kwa mfumo wa sasa wa tiketi za kawaida na kuanza kutumika tiketi za elektroniki.
Ukurasa wa 29 wa ripoti hiyo yenye jumla ya kurasa 95 na viambatanisho tisa unasema: “Baadhi ya watendaji wakuu ndani ya TFF wanajihusisha na kuhujumu mapato kwa kuchapisha tiketi za ziada na kuziuza kwanza.”
“Kuna tiketi nyingi za kughushi/ bandia zinazotengezwa kwa ushirikiano kati ya viongozi wa soka na wapenzi wa mpira wa miguu. Viongozi hawa ni wale waliokaa madarakani kwa muda mrefu,” inaeleeza zaidi ripoti hiyo katika ukurasa wa 30.
Januari mwaka huu mmoja wa maafisa wa CRDB (jina linahifadhiwa) aliliambia gazeti hili kuwa benki yao imejipanga vyema kuendesha mfumo wa tiketi za elektroniki lakini wanacheleweshwa na TFF.
Miongoni mwa madhara yatokananyo na kutotumika kwa tiketi za elektroniki ni kutoa fursa kwa baadhi ya watu kutengeneza na kuuza tiketi bandia.
Pia kutotumia tiketi za elektroniki wakati mwingine kumekuwa kukichangia baadhi ya mashabiki wanaokwenda viwanjani kukosa tiketi ama kuuziwa tiketi kwa bei tofauti na iliyopendekezwa na wasimamizi wa soka letu (TFF).
Mfano mzuri ni mechi ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara ya Yanga dhidi ya Azam iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Katika mechi iliyomalizika kwa Yanga kuibuka na ushindi wa 1-0 baadhi ya mashabiki waliofika uwanjani kununua tiketi kwenye mabasi madogo ya TFF, walirudi nyumbani pasipo kuangalia mechi hiyo baada ya tiketi zilizokuwa zimeaandaliwa kumalizika.
Aidha, kumekuwa kukijitokeza tatizo la kuingiza idadi kubwa ya watu ukilinganisha na uwezo wa viwanja vyetu.
Tukumbuke idadi ya watu walioingia kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kushuhudia mechi ya kufunga msimu wa 2012/13 ya Simba dhidi ya Yanga (Mei 18) na mechi ya kuwania kufuzu kushiriki fainali zijazo za Kombe la Dunia ya Taifa Stars dhidi ya Ivory Coast.
CHANZO;IPPMEDIA&NIPASHE
No comments :
Post a Comment